UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

Jessica Mshama atoa pongezi kwa Viongozi wa Vijana Walioshiriki Katika Kikao Kazi cha UVCCM Mkoa wa Dodoma

07 Dec, 2025 18 Machapisho
DODOMA, TANZANIA — Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imetoa shukrani na pongezi za kipekee kwa viongozi wote wa vijana waliohudhuria kikao kazi cha Umoja wa Vijana kilichofanyika jijini Dodoma tarehe 7 Desemba 2025  ambapo washiriki walijadiliana juu ya mustakabali wa vijana, amani ya nchi na maendeleo ya taifa.

Akitoa kauli hiyo kwa niaba ya idara, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM, Ndugu Jessica Mshama, alisema kuwa mwitikio mkubwa wa viongozi wa vijana kutoka ngazi ya Taifa, Makatibu wa Vijana, Makatibu wa Hamasa, pamoja na viongozi wa Seneti, umeonyesha kwa mara nyingine dhamira njema ya kulinda na kuendeleza misingi ya umoja, uzalendo, amani na maendeleo nchini.

 “Ushiriki wenu umetudhihirishia kwamba tunabeba dhamana ya vijana wa Taifa kwa umoja, uzalendo na kwa dhamiri ya kutumikia nchi yetu. Mmekuwa mfano wa uongozi makini unaoenzi misingi ya maadili, mshikamano na uwajibikaji,” alisema Jessica Mshama.

Aidha, alisisitiza kuwa UVCCM inaendelea kuthamini mawazo, mchango na mjadala mzito uliotolewa na vijana katika kikao hicho, akisema kuwa nguvu, nidhamu na ari ya viongozi hao imeendelea kuipa nguvu Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi kusukuma mbele ajenda za maendeleo na ustawi wa vijana.

 “Nawakumbusha kuendelea kusimama imara, kutekeleza kwa ukamilifu maelekezo yote tuliyopokea, na kuendeleza hamasa za amani na maendeleo popote tulipo. Sisi ni viongozi wa fikra, viongozi wa maendeleo, na viongozi wa amani,” aliongeza.

Katika salamu zake, Jessica aliwapongeza pia viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi kwa usimamizi bora wa jumuiya, akitoa shukrani za pekee kwa Mgeni Rasmi wa kikao, Ndugu Kenani Kihongosi, kwa uwepo na mchango wake katika majadiliano.

Vilevile, alitoa pongezi maalumu kwa Mwenyekiti wa UVCCM Tanzania  Ndugu Comrade Kawaida(MCC) kwa uongozi wake imara na mwanga kwa vijana wanaoendeleza kazi za CCM na serikali.

Katika kumalizia, Katibu huyo aliomba vijana waendelee kulinda misingi ya amani, ustaarabu na maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa UVCCM itaendelea kuwa jumuiya  imara  katila kulinda maslahi ya vijana na mustakabali wa Tanzania.

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA,” alihitimisha.