UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

DKT.MWINYI ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA BIASHARA ENEO LA DARAJANI

16 Oct, 2025 32 Machapisho
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema lengo la Serikali ni kuendelea kuliimarisha eneo la Darajani na kujenga miundombinu zaidi ili wafanyabiashara wapate maeneo mazuri na ya kisasa ya kufanyia biashara.

Dkt. Mwinyi ameeleza kuridhishwa na hali ya ufanyaji biashara katika eneo hilo, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara ili kukuza uchumi wa wananchi na wa Taifa kwa ujumla.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 16 Oktoba 2025, alipokutana na wafanyabiashara na wajasiriamali wa soko la Darajani, ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa kampeni zake za kuomba kura na kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi.

Amesema Serikali imepanga pia kujenga maegesho katika eneo la Malindi ili kuondoa utaratibu wa kuegesha magari kiholela. Aidha, ameeleza kuwa mradi mkubwa wa BIG Z, utakaojenga maduka pembezoni mwa barabara, unakuja na utaongeza haiba na mvuto wa eneo la mjini.

Akizungumzia barabara ya Malindi hadi Mnazi Mmoja, amesema itapanuliwa kuwa ya njia nne sambamba na ujenzi wa maegesho mapya katika eneo la Malindi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa katika awamu ijayo, Serikali itatenga fedha zaidi kwa ajili ya mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali, hasa wale waliowahi kukopa na kurejesha mikopo yao kwa wakati, ili kuwaongezea mtaji na nguvu ya kiuchumi.

Kuhusiana na kodi, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itakaa na Chama Cha Mapinduzi kujadiliana juu ya namna bora ya kutatua changamoto hizo na kuona uwezekano wa kupunguza kodi kwa wafanyabiashara. Pia, ameliagiza Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuweka transfoma mpya katika eneo la Darajani ili kumaliza tatizo la umeme linalowakabili wafanyabiashara.

Ameomba wananchi na wafanyabiashara kumpa kura nyingi katika uchaguzi ujao ili aendelee kutekeleza ahadi anazozitoa sasa, pamoja na kuimarisha amani, umoja na maendeleo kupitia uongozi wa Chama Cha Mapinduzi.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wa Darajani Souk wamemshukuru Dkt. Mwinyi kwa mageuzi makubwa yaliyofanyika katika eneo hilo, ikiwemo kuboreshwa kwa mazingira ya biashara, kurejeshwa kwa kituo cha daladala na kuboreshwa kwa bustani, hatua zilizosaidia kuongeza idadi ya wanunuzi.

Wamesema wanathamini jitihada za Dkt. Mwinyi katika kubadilisha sura ya Zanzibar na kuwajali wafanyabiashara wadogo na wa kati, huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono katika juhudi zake za kuleta maendeleo endelevu nchini.