Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)
KAWAIDA: VIJANA JIPANGENI KUNUFAIKA NA MIKOPO YA SERIKALI | UVCCM
Habari za Kitaifa (UVCCM) Kipaumbele

KAWAIDA: VIJANA JIPANGENI KUNUFAIKA NA MIKOPO YA SERIKALI

18 May, 2026 Admin User 32 views min read

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mohammed Ali Kawaida, amewataka vijana nchini kuendelea kujipanga katika vikundi, kuandaa maandiko yenye ubora na kutumia ipasavyo fursa za mikopo zinazotolewa na Serikali ili kujikwamua kiuchumi.

Kawaida amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutenga fedha za mikopo kwa makundi mbalimbali ya kijamii, hususan vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuwasaidia kupata mitaji ya kuanzisha shughuli za maendeleo na uzalishaji mali.

Akizungumza jana mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi iliyoanza rasmi leo, Kawaida alisema kumekuwa na upotoshaji kutoka kwa baadhi ya viongozi wa upinzani wanaodai kuwa vijana hawapati mikopo hiyo, jambo ambalo alisisitiza kuwa si la kweli.

Alieleza kuwa vijana wengi tayari wananufaika na mikopo hiyo nchini, akitoa mfano wa baadhi ya vijana wa Mkoa wa Mtwara waliopata mkopo wa Shilingi milioni 50 kwa ajili ya shughuli za uzalishaji wa tofali.

“Hivi karibuni nimemsikia mwenyekiti mmoja wa chama cha upinzani akizungumza mara kwa mara kupitia vyombo vya habari akiikosoa Wizara ya Vijana kwa kudai hakuna kinachofanyika. Nikasema nipelekwe nikajionee kwa ushahidi kile ambacho Serikali ya Dkt. Samia inafanya. Wengine wanabaki na makaratasi, lakini mimi nimekuja kushuhudia utekelezaji wenyewe,” alisema Kawaida.

Aidha, alisema baadhi ya viongozi wa vijana kutoka vyama vya upinzani wamekuwa wakitoa taarifa zisizo na ushahidi kuhusu mikopo hiyo badala ya kufika maeneo ya wananchi na kujionea namna vijana wanavyonufaika na programu za uwezeshaji kiuchumi zinazotekelezwa na Serikali.

Katika hatua nyingine, Kawaida alisema ziara yake katika Mkoa wa Mtwara itahusisha wilaya zote za mkoa huo, huku lengo kuu likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 pamoja na kubaini watendaji wanaokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisisitiza kuwa hatakuwa na uvumilivu kwa watendaji wazembe wanaochelewesha utekelezaji wa majukumu yao, akieleza kuwa wananchi wameendelea kuiamini Serikali kutokana na juhudi zake za kuwaletea maendeleo.

“Kwa lugha nyepesi naweza kusema nimekuja kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi mkoani Mtwara, lakini kwa lugha nyingine ni kwamba nimekuja kushughulika na watendaji wazembe wanaokwamisha utekelezaji wa Ilani yetu,” alisema Kawaida.