Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)
KATIBU MKUU UVCCM HALID MWINYI: “VIJANA TUITUNZE AMANI NA TUPENDANE | UVCCM
Habari za Kitaifa (UVCCM) Kipaumbele

KATIBU MKUU UVCCM HALID MWINYI: “VIJANA TUITUNZE AMANI NA TUPENDANE

09 May, 2026 Admin User 40 views min read

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Halid Mwinyi, amewataka vijana nchini, hususan Gen Z, kuendelea kuitunza amani ya Tanzania, kupendana na kushiriki shughuli za maendeleo badala ya migawanyiko na vurugu.
Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Mei 09, 2026 wakati akifunga mashindano ya mpira wa miguu ya Sodo Cup yaliyofanyika Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, ambapo alisema vijana wameamua kusema “Never Again” na kutorudia tena kushiriki matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
“Vijana tuitunze amani tupendane. Jana Mheshimiwa Rais akiwa Dodoma vijana walisema ‘Never Again’, hatutofanya tena. Naomba wakazi wa Dar es Salaam tumuunge mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mwinyi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni, Abdulrahman Abdallah Kassim, alisema mashindano hayo yaliyodumu kwa mwezi mmoja yalilenga kuonesha namna CCM inavyoendelea kuungwa mkono na vijana pamoja na wananchi wa Kinondoni.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na UVCCM Kinondoni yalihitimishwa kwa mshindi wa kwanza kujinyakulia kombe na shilingi milioni 3, mshindi wa pili milioni 1.4 na mshindi wa tatu milioni 1, huku Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Ali Kawaida, kupitia kwa Katibu Mkuu Halid Mwinyi, akiongeza zawadi ya shilingi laki 3 kwa timu zilizoshika nafasi tatu za juu.