Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)
Rais Dkt.Samia: Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa | UVCCM
Habari za Kitaifa (UVCCM) Kipaumbele

Rais Dkt.Samia: Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa

26 Apr, 2026 Admin User 51 views min read

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa vijana ndio nguvu kazi kuu ya taifa kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi 2022, akibainisha kuwa mustakabali wa nchi unategemea namna watakavyoshiriki katika ujenzi wa uchumi, siasa na jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika Kongamano la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) lililofanyika Tunguu, Zanzibar, Rais Samia alieleza kuwa Serikali imechukua mkakati mahsusi wa kujenga mazingira wezeshi kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kuhakikisha vijana wanakuwa washiriki hai katika michakato ya uamuzi na uongozi wa taifa.

Alifafanua kuwa dhamira ya Serikali si tu kuwaandaa vijana, bali kuwapa nafasi halisi katika ngazi za juu za uamuzi. Hili, kwa mujibu wake, linajidhihirisha wazi katika muundo wa sasa wa Serikali ambapo sehemu kubwa ya mawaziri na manaibu mawaziri ni vijana. Aliongeza kuwa hata katika vikao vya Baraza la Mawaziri, zaidi ya robo tatu ya wajumbe wako chini ya umri wa miaka 50, hali inayoakisi mwelekeo wa kimkakati wa kizazi kipya kupewa dhamana ya kuendesha Serikali.
“Nchi hii kwa sasa inaendeshwa kwa nguvu kubwa ya vijana; sisi tuliopo katika ngazi za juu tunabaki na jukumu la kutoa mwelekeo wa kimkakati, kulinda misingi ya sera na kufanya maboresho ya kisheria pale inapobidi,” alisisitiza Rais Samia.
Aidha, alibainisha kuwa hatua hiyo si ya bahati mbaya, bali ni utekelezaji wa makusudi wa dira ya maendeleo ya taifa pamoja na maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ambayo inaelekeza Serikali zote mbili kuwekeza kwa makusudi katika kuwaendeleza vijana kama injini ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Kwa kuhitimisha, Rais Samia alisisitiza kuwa fursa zilizopo katika sekta mbalimbali zinahitaji kuambatana na uwajibikaji, nidhamu na uzalendo, akiwataka vijana kuzitumia kwa ufanisi ili kuharakisha maendeleo jumuishi na endelevu ya taifa.