UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

UVCCM Mufindi yaadhimisha Miaka 49 ya CCM kwa Baraza maalum, yasifu Mchango wa Vijana katika kutafuta ushindi kwa CCM

31 Jan, 2026 10 Machapisho
Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Mufindi umeanza maadhimisho hayo kwa kufanya baraza maalum lenye lengo la kuwapongeza na kuwashukuru vijana wa chama kwa mchango wao mkubwa katika kazi ya kutafuta kura wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.
Baraza hilo lilifanyika likihusisha viongozi na vijana wa chama, ambapo Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Ndugu Agrey Tonga, alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo muhimu la kutafakari mchango wa vijana katika ushindi wa CCM na mustakabali wa taifa.
Akizungumza katika baraza hilo, Ndugu Agrey Tonga aliwasisitiza vijana wa CCM kuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira kwa vitendo, akibainisha kuwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji ushiriki wa vijana kama mabalozi wa mazingira kuanzia ngazi ya familia hadi jamii kwa ujumla.
“Vijana wa CCM mna wajibu mkubwa wa kuwa mfano katika kulinda mazingira, kupanda miti, kutunza vyanzo vya maji na kuelimisha jamii juu ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Hili ni jukumu la kizalendo na la kizazi,” alisema Ndugu Agrey.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa UVCCM Mkoa alitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliangalia kundi la vijana kwa jicho la tatu, hususan kwa kuanzisha Wizara maalum inayoshughulikia masuala ya vijana ndani ya Baraza la Mawaziri, hatua aliyoitaja kuwa ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya Serikali katika kuwawezesha vijana kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Aliongeza kuwa uwepo wa wizara hiyo ni fursa adhimu kwa vijana kujipanga, kushiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo na kutumia sera na programu za Serikali kwa manufaa ya taifa.
Kaulimbiu ya baraza hilo ilisisitiza mshikamano na utulivu wa nchi kwa maendeleo, ambapo vijana walikumbushwa kuwa umoja na amani ni nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania.
“Tumechagua Umoja na Amani kwa Maendeleo ya Taifa.”