UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

DKT. SAMIA AONGOZA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM TAIFA, ZANZIBAR

25 Jan, 2026 33 Machapisho
Zanzibar | Januari 25, 2026
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Zanzibar tarehe 25 Januari 2026.

Katika kikao hicho, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilipitia, kujadili na kufanya uteuzi wa wagombea mbalimbali wa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi wanaotokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kwa mujibu wa Katiba, kanuni na taratibu za Chama.

Kwa upande wa uteuzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wanaotokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Tanzania Bara, Kamati Kuu iliwateua Paul Christian Makonda na Livingstone Joseph Lusinde kwa nafasi za wanaume, pamoja na Asia Abdulkarim Halamga kwa nafasi ya mwanamke. Aidha, kutoka upande wa Zanzibar, Kamati Kuu ilimchagua Khamis Mussa Omar kwa nafasi ya mwanaume na Tauhida Cassian Galos kwa nafasi ya mwanamke kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Vilevile, Kamati Kuu ilimteua Agnes Elias Hokororo kuwa Katibu wa Wabunge Wote wa CCM, huku Najma Murtaza Giga, Deodatus Philipo Mwanyika na Cecilia Daniel Pareso wakiteuliwa kuwa Wenyeviti wa Bunge kwa nafasi tatu zilizotengwa.

Kwa upande wa uteuzi wa wagombea wanaotokana na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Kamati Kuu ya CCM Taifa iliwateua Said Ali Juma na Hamza Hassan Juma kwa nafasi za wanaume, pamoja na Lela Muhamed Mussa kwa nafasi ya mwanamke, kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Aidha, Kamati Kuu iliwateua Bakar Hamad Bakar, Dkt. Shaame Ali Ali na Simai Mohammed Said kuwa Wawakilishi wa CCM watakaoingia Bungeni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi za wanaume, huku Fatma Ramadhan Mandoba akiteuliwa kwa nafasi ya mwanamke. Katika uteuzi huo huo, Machano Othman Said aliteuliwa kuwa Katibu wa Wawakilishi Wote wa CCM, wakati Mahmoud Omar Hamad na Hudhaima Mbarak Tahir wakiteuliwa kuwa Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi.

Kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Peramiho, Mkoa wa Ruvuma, Kamati Kuu, kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 105(7)(f) ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977, Toleo la Julai 2025, ilimteua Dkt. Lazaro Killian Komba kuwa Mgombea wa CCM katika uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Peramiho lililopo Wilaya ya Songea Vijijini.
Maamuzi yaliyofikiwa katika kikao hiki yanaendelea kuimarisha misingi ya uongozi, mshikamano na uwakilishi mpana ndani ya Chama Cha Mapinduzi, sambamba na kulinda misingi ya Katiba ya Chama na maslahi mapana ya Taifa.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI