Dodoma | Januari 24, 2026
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kupitia jukwaa la mtandao UVCCM e-Talk, tarehe 24 Januari 2026, kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 2:00 usiku, uliendesha mjadala mpana wa kitaifa uliowakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kujadili nafasi na mchango wa vijana katika siasa na ujenzi wa taifa.
Mjadala huo ulilenga kuibua fikra, kujenga uelewa wa pamoja na kuhamasisha ushiriki chanya wa vijana katika masuala ya kitaifa, hususan katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa na kiteknolojia.
USHIRIKI WA VIJANA KATIKA SIASA NA UJENZI WA TAIFA
Mjadala ulijikita katika mada kuu *“Ushiriki wa Vijana katika Siasa na Ujenzi wa Taifa”*, sambamba na mada ndogo zilizogusa matumizi chanya ya mitandao ya kijamii, maandalizi ya kizazi cha Gen Z kuwa viongozi wa leo na kesho ndani ya UVCCM, pamoja na kuimarisha siasa za maadili katika enzi ya mitandao ya kijamii.
Mada hizo ziliwasilishwa na Ndugu Jessica Mshama, Katibu wa Hamasa na Chipukizi UVCCM Taifa, pamoja na Ndugu Agrey Tonga, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa.
VIJANA NA FURSA ZA ELIMU
Katibu wa Hamasa na Chipukizi UVCCM Taifa, Ndugu Jessica Mshama, alisisitiza kuwa vijana si watazamaji wa maendeleo, bali ni nguzo kuu ya maamuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya taifa.
Alieleza kuwa demokrasia ya kweli haiwezi kukamilika bila ushiriki wa vijana katika hatua zote, kuanzia upangaji wa sera hadi utekelezaji wake. Alibainisha pia kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kufungua milango ya fursa kwa vijana, hususani katika sekta za elimu, ujasiriamali, teknolojia na ajira. Alitaja miongoni mwa fursa hizo Samia Scholarship na programu nyingine za kitaifa zinazowasaidia vijana kupata elimu bora na usaidizi wa kifedha.
Ndugu Jessica pia aliongeza wito kwa vijana:-
“Wakati mwingine vijana tumekuwa tukitamani nafasi kubwa tu bila kujua kuwa katika kuisaidia jamii au kuonyesha uwezo wetu tunaweza kuanza na nafasi hata ndogo kwenye jamii inayotuzunguka na kuwa daraja bora katika jamii yetu.”
MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA NA UCHUMI WA VIJANA
Ndugu Jessica aliwahamasisha vijana kuchangamkia mapinduzi ya teknolojia kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa, akisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Unde (Artificial Intelligence (AI)), katika uundaji wa maudhui, biashara za kidijitali na ubunifu unaochochea ukuaji wa uchumi.
Alitolea mfano wa mataifa yaliyofanikiwa, kama Rwanda na Singapore, ambayo yaliwekeza kwa makusudi katika elimu, sayansi na teknolojia kwa vijana wao, jambo lililoyawezesha kujenga uchumi imara na ushindani wa kimataifa. Alisisitiza kuwa Tanzania ina fursa hizo, kama zinavyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, endapo vijana watazichangamkia kwa vitendo.
MSHIKAMANO WA KITAIFA NA MAADILI YA VIJANA
Katika mjadala huo, Ndugu Agrey Tonga alisisitiza kwa nguvu kuwa vijana wanapaswa kufanya matendo yao yawe kielelezo cha maadili:
*“Kijana lazima uyaishi matendo yako kwa kuzingatia maadili ili kuongeza nguvu ya ushawishi kwa vijana unaowaongoza. Hakuna taifa linalodumu kwa misingi ya matusi na kejeli.”*
Pia alisisitiza:
“Tanzania ya kesho haitajengwa na watu wengine, bali tutaijenga sisi wenyewe.”
Ilisisitizwa kuwa kulinda mshikamano wa kitaifa, kuvuka mipaka ya kikabila, kidini na kieneo, na kulinda maslahi ya vizazi vijavyo ni jukumu la kizazi cha sasa.
Ndugu Jessica Mshama alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuanzisha Wizara ya Vijana, hatua ambayo imeiweka vizazi vipya katikati ya ajenda za kitaifa.
MATUMIZI CHANYA YA MITANDAO YA KIJAMII
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa alibainisha kuwa mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu ya demokrasia, inayowezesha vijana kuhoji, kujifunza, kuwasiliana na kusambaza taarifa. Hata hivyo, alionya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao kwa kueneza upotoshaji, udini, ukabila na lugha za chuki. Alisisitiza kuwa uhuru wa maoni unapaswa kuambatana na uwajibikaji, hoja, heshima na kulinda amani ya taifa.
*GEN Z: VIONGOZI WA LEO NA KESHO*
Mjadala huo uliweka wazi kuwa vijana wengi tayari ni viongozi wa leo, na kwamba dhana ya muda mrefu ya *“vijana ni viongozi wa kesho”* inahitaji tafsiri mpya. Ilisisitizwa kuwa uongozi bora unahitaji mchanganyiko wa maarifa, maadili, uadilifu na heshima, na kizazi cha Gen Z kina wajibu mkubwa wa kulinda misingi ya taifa.
HITIMISHO
UVCCM e-Talk imeonesha kuwa vijana wa Tanzania wana uelewa mpana wa masuala ya taifa, wako tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi, siasa za maadili na wanatambua kuwa maendeleo hayawezi kupatikana kwa makelele ya mitandaoni pekee. Ushiriki wa vitendo, ubunifu, maadili na uzalendo ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Mjadala ulihitimishwa kwa wito kwa vijana kuendelea kushirikiana, kutumia fursa zilizopo, na kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani, umoja na maendeleo ya Tanzania.
#KaziNaUtuTunasongaMbele