UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

PPRA YAWAJENGEA UWEZO VIJANA KUSHIRIKI UNUNUZI WA UMMA

24 Jan, 2026 28 Machapisho
Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuwajengea uwezo vijana ili washiriki kikamilifu katika mifumo ya ununuzi wa umma, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukuza ushiriki wa vijana katika uchumi wa taifa.

Hayo yameelezwa leo tarehe 24 Januari, 2026 na Afisa Ugavi wa PPRA, Ndugu Glory Minja, wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la UNI-Summit Life In and After Campus, lililowakutanisha maelfu ya vijana kutoka vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Akizungumza katika kongamano hilo, Ndugu Minja amesema kuwa vijana ni kundi kubwa na lenye nguvu katika jamii ya Tanzania, hivyo Serikali kupitia PPRA imeweka mikakati ya makusudi ya kuwapa upendeleo ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya ununuzi wa umma. Alisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuleta haki, usawa na ujumuishi wa maendeleo ya kiuchumi kwa makundi yote ya jamii.

Fursa ya asilimia 30 kwa makundi maalum
Aidha, imeelezwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa maagizo kwa taasisi zote nunuzi kutenga asilimia 30 ya mpango wao wa ununuzi wa mwaka kwa ajili ya makundi maalum, yakiwemo vijana, ili kuwawezesha kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa bidhaa, kazi na huduma kwa Serikali.
Hatua hiyo inalenga kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, kuongeza ushindani wenye tija, pamoja na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika mfumo wa ununuzi wa umma nchini.
Kongamano la UNI-Summit limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwapa vijana elimu ya vitendo kuhusu fursa zilizopo wakati wa masomo na baada ya kuhitimu, hususan katika maeneo ya ajira, ujasiriamali na ushiriki katika miradi ya maendeleo ya taifa.
#KaziNaUtuTunaSongaMbele
#UniSummitLifeInAndAfterCampus