UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

SERIKALI YATAJA MALENGO YA SERA YA MAENDELEO YA VIJANA (2007 – 2024)

24 Jan, 2026 46 Machapisho
Dodoma. Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana imeendelea kuweka msisitizo katika uwekezaji wa kimkakati kwa vijana, kwa kueleza maeneo muhimu ya Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, Toleo la Mwaka 2024, yenye lengo la kumwezesha kijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Maelezo hayo yametolewa katika Kongamano la UNI-Summit Life In & After Campus, lililowakutanisha maelfu ya vijana kutoka vyuo vya kati na vyuo vikuu mkoani Dodoma. Maofisa kutoka Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana waliwasilisha mada inayochambua kwa kina fursa na mwelekeo mpya wa sera hiyo kwa vijana wa Tanzania.
Maeneo manne ya kimkakati kwa maendeleo ya vijana
Katika wasilisho lao, maofisa hao walitaja maeneo manne muhimu yanayolenga kumjenga kijana kielimu, kiuchumi na kiteknolojia ili aweze kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo.
Eneo la kwanza ni Elimu na Ujuzi kwa Vijana, likilenga kukuza elimu na ujuzi unaoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira. Serikali inalenga kuhakikisha vijana wanapata maarifa yanayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa kwa ufanisi.
Eneo la pili ni Uvumbuzi na Ubunifu kwa Vijana, likiwa na dhamira ya kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana katika nyanja mbalimbali ikiwemo sayansi, teknolojia, sanaa na ujasiriamali.
Eneo la tatu ni Vijana na Mapinduzi ya Kidijitali, ambapo mkazo unawekwa katika kuimarisha ujuzi wa kidijitali, kuongeza ufikivu wa teknolojia, pamoja na kuhakikisha vijana wanapata bidhaa na huduma za kidijitali kwa gharama nafuu.
Eneo la nne ni Ajira kwa Vijana, likilenga kukuza fursa za ajira kwa njia ya kujiajiri au kuajiriwa, sambamba na kuweka mazingira rafiki kwa vijana kushiriki katika uchumi wa vijana.
Mada hiyo iliwasilishwa na Afisa Mwandamizi wa Maendeleo ya Vijana, Nasibu Mwaifunga, pamoja na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Ofisi ya Rais  Maendeleo ya Vijana, Edward Haule. Wote walisisitiza umuhimu wa vijana kuitumia sera hiyo kama nyenzo ya kujitambua, kupanga mustakabali wao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Kongamano la UNI-Summit limeendelea kuwa jukwaa muhimu la majadiliano kuhusu maisha ya mwanafunzi akiwa chuoni na baada ya kuhitimu, likitoa nafasi kwa vijana kupata elimu ya sera, fursa na mwelekeo wa maendeleo ya taifa.
#KaziNaUtuTunaSongaMbele
#UniSummitLifeInAndAfterCampus