UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

Kihongosi Apeleka Tabasamu Mashina ya CCM Singida

20 Jan, 2026 21 Machapisho
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Kenani Laban Kihongosi, ameendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Singida, ikiwa ni siku ya pili ya ziara hiyo, ambapo leo amepokelewa rasmi Wilaya ya Singida.
Mara baada ya mapokezi, Ndg. Kihongosi alitembelea Shina Namba 1, Tawi la Kibaoni – Singida Mjini, ambapo alipandisha bendera ya Chama Cha Mapinduzi katika shina hilo, ikiwa ni ishara ya kuimarisha mshikamano, uzalendo na uhai wa Chama katika ngazi ya mashina.
Katika ziara hiyo, Shina la Kibaoni liliwasilisha pongezi za dhati kwa Mwenyekiti wa Chama Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kukijenga na kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi pamoja na kuwajali mabalozi na wanachama wote wa Chama nchini.
Aidha, shina hilo liliwasilisha changamoto mbalimbali, zikiwemo ucheleweshaji wa upatikanaji wa kadi za kielektroniki na masuala ya ulinzi. Akijibu risala hiyo, Ndg. Kihongosi aliwahakikishia wanachama kuwa kadi za kielektroniki tayari zimeshakamilika na zitawafikia wanachama husika hivi karibuni.
Ndg. Kihongosi aliwahimiza wanachama kuendelea kutembea kifua mbele, wakijivunia Chama chao, akisisitiza kuwa CCM ni chama kinachotekeleza ahadi zake kwa vitendo na kinachowajali wananchi wake bila ubaguzi.
Ziara ya Ndg. Kihongosi inaendelea kuwa chachu ya kuimarisha itikadi, mafunzo ya kisiasa na mshikamano wa wanachama, huku ikidhihirisha dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ya kuendelea kujijenga, kujisahihisha na kubaki kuwa nguzo ya amani, umoja na maendeleo ya Taifa.
Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.