UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

KATIBU WA NEC KENANI KIHONGOSI ATANGAZA ZIARA YA KITAIFA YA KUSIMAMIA MIRADI, KUSIKILIZA KERO NA KUIMARISHA UMOJA WA TAIFA

17 Jan, 2026 27 Machapisho
Dodoma, Januari 17, 2026
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kudhihirisha kwa vitendo falsafa yake ya kuwa chama cha wananchi, baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Kenani Labani Kihongosi, kutangaza kuanza kwa ziara ya kitaifa ya kichama itakayohusisha mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ukumbi wa Jakaya Convention Centre (JCC) jijini Dodoma, Ndugu Kihongosi amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, pamoja na kuendelea kuilinda amani na umoja wa Taifa.
Amesema CCM haiwezi kuwa chama cha watu endapo kitaongoza kwa kusikiliza taarifa za mezani pekee, bali lazima kiwe karibu na wananchi na kuwasikiliza moja kwa moja.
“Kama chama, tuna wajibu wa kwenda kuisimamia Serikali. CCM ni chama cha watu, na hatuwezi kuongoza kwa kusikia taarifa za mezani pekee. Lazima tushuke kwa wananchi, tusikilize kero zao na kuzitatua,” alisema Ndugu Kihongosi.

Amefafanua kuwa CCM ni chama cha kimaendeleo na kijamii, kinachojengwa juu ya misingi imara ya amani, umoja, mshikamano na kulinda utu wa Mtanzania, misingi ambayo imekiwezesha chama hicho kuiongoza Tanzania kwa uthabiti na amani kwa muda mrefu.
Ameongeza kuwa chama hicho kinatanguliza maslahi ya Taifa kuliko maslahi binafsi au ya makundi, na hakijengi taifa kwa chuki, migawanyiko au misingi ya kudhoofisha umoja wa wananchi.
“CCM ni chama kinachopenda amani, kinacholinda utu wa Mtanzania na kinachotanguliza maslahi ya Taifa mbele ya maslahi binafsi au ya makundi. Taifa linajengwa kwa umoja na mshikamano, si kwa migawanyiko,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Katibu huyo wa NEC amepongeza uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan kwa hatua yake ya kukutana na Mabalozi wa Tanzania wanaoziwakilisha nchi mbalimbali duniani katika kikao cha kufungua mwaka, akisema hatua hiyo imeongeza hadhi na heshima ya Tanzania kimataifa.
Amesema uongozi wa Rais Samia umeendelea kuimarisha diplomasia ya nchi, kuijenga Tanzania yenye heshima, sauti na ushawishi katika medani za kimataifa, jambo linalowapa faraja na matumaini wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla.
Kupitia ziara hiyo ya kitaifa, CCM pia itafanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Samia, kusimamia maslahi ya wananchi, na kuhakikisha hakuna upotoshaji wowote unaofanywa dhidi ya juhudi za Serikali na chama katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Ziara hiyo inatajwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa CCM wa kuendelea kujijenga kama chama cha wananchi, kinachosikiliza, kinachojifunza kutoka kwa wananchi wake, na kinachotatua changamoto kwa vitendo.