UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

INJINI YA CCM IPO MASHINANI; DKT. MIGIRO ASISITIZA UONGOZI WA KARIBU NA WANANCHI

13 Jan, 2026 37 Machapisho
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, amesema kuwa mashina ndiyo injini halisi ya uhai, uhalali na maendeleo ya Chama Cha Mapinduzi, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli ya wananchi huanzia katika ngazi za chini za chama.
Dkt. Migiro ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Mabalozi wa Mashina wa CCM Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, katika mkutano uliokuwa ni hitimisho la ziara yake ya kuimarisha chama Mkoa wa Dar es Salaam, chini ya kaulimbiu “Shina Lako Linakuita”.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Migiro amesema mashina ndiyo ngazi ya kwanza inayowaunganisha wananchi moja kwa moja na Chama, kwani ndiko wanakotoka wananchi wenyewe na ndiko changamoto zao halisi zinapojadiliwa, kusikilizwa na kufanyiwa kazi.
Amesisitiza kuwa uhalali wa uongozi wa CCM unaonekana wazi kupitia ukaribu wake na wananchi katika mashina, hivyo viongozi wa ngazi za Mashina, Matawi na Kata wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanakuwa macho, wasikivu na wanashiriki kikamilifu katika kusimamia na kunufaika na maendeleo yanayotekelezwa ndani ya chama na serikalini.
Dkt. Migiro ameongeza kuwa maendeleo ya kisiasa na maendeleo ya kijamii hayawezi kutenganishwa, akieleza kuwa mashina imara huwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji, jambo linaloongeza imani ya wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi.
Aidha, amewataka Mabalozi wa Mashina kuendelea kupandisha na kulinda bendera ya chama katika maeneo yao, kwa kuwa wao ni mabalozi wa kwanza wa sera, maadili na mwelekeo wa CCM katika jamii.
Katibu Mkuu huyo ameweka bayana kuwa CCM imejengwa juu ya misingi ya umoja wa kitaifa, kwa kuwashirikisha Wanachama na wasio Wanachama katika shughuli za maendeleo, bila kujali tofauti za kikanda, kijamii au kiitikadi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Migiro amesema Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Mabalozi wa Mashina nchi nzima, akisisitiza kuwa chama kitaendelea kuwajali, kuwathamini na kuwaunga mkono, kutokana na mchango wao mkubwa katika kuimarisha chama kuanzia ngazi ya chini kabisa.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa nguvu ya CCM iko kwa wananchi, na wananchi hao wanapatikana mashinani, hivyo kuimarisha mashina ni kuimarisha chama na mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
#ShinaLakoLinakuita