UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

ZANZIBAR KUANZA USAFIRI WA MABASI YA UMEME MWISHONI MWA FEBRUARI 2026

09 Jan, 2026 19 Machapisho
 Unguja – Zanzibar
Zanzibar inatarajiwa kuanza rasmi usafiri wa umma wa kutumia mabasi ya umeme mwishoni mwa mwezi Februari, 2026, hatua itakayofungua ukurasa mpya katika sekta ya usafiri wa kisasa na rafiki kwa mazingira visiwani humo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mradi huo utaanza kutekelezwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, na unalenga kupunguza msongamano wa magari barabarani, kuboresha uhakika na ubora wa safari kwa wananchi, pamoja na kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya nishati ya mafuta.
Mradi huu unatekelezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa ushirikiano na Kampuni ya GRT Limited, baada ya pande hizo mbili kuingia mkataba rasmi wa utekelezaji. Mabasi hayo ya umeme yataendeshwa kwa mfumo maalum wa kisasa na kutumia vituo vya kisasa vilivyopangwa katika maeneo mbalimbali, huku yakitembea katika barabara za kawaida.

Utekelezaji kwa Awamu Tatu
Mradi wa mabasi ya umeme utafanyika kwa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha Mkoa wa Mjini Magharibi na itapita katika njia kuu zifuatazo:
  • Uwanja wa Ndege – Malindi
  • Buyu – Chukwani – Mnazi Mmoja – Malindi
Katika mpango huo, Kituo cha Kijangwani kitakuwa kiunganishi kikuu cha mabasi yote, huku vituo vingine muhimu vikiwekwa ndani ya Uwanja wa Ndege na Bandari ya Malindi, hatua itakayorahisisha muingiliano wa usafiri wa anga, majini na barabara.
Mabasi ya umeme yanatarajiwa kuanza kuwasili Zanzibar mwanzoni mwa mwezi Februari, 2026, kabla ya kuanza kutoa huduma rasmi mwishoni mwa mwezi huo.

Hatua ya Maendeleo Endelevu
Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuimarisha maendeleo ya miundombinu na huduma za kijamii, sambamba na kuhimiza matumizi ya nishati safi na usafiri rafiki kwa mazingira.

Mradi wa mabasi ya umeme unatarajiwa kuwa kichocheo cha mageuzi ya usafiri wa umma Zanzibar, kuongeza ajira, kuboresha huduma kwa wananchi na kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa matumizi ya teknolojia ya kijani barani Afrika.