UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

MWENYEKITI KAWAIDA AONGOZA MATEMBEZI YA KUADHIMISHA MIAKA 62 YA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR, KUSINI PEMBA

09 Jan, 2026 59 Machapisho
Na Mwandishi wetu, Kusini Pemba.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndugu Mohammed Ali Kawaida (MCC), leo Ijumaa tarehe 09 Januari, 2026 ameongoza maelfu ya vijana katika Matembezi ya Amani ya kuadhimisha Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yaliyofanyika katika Mkoa wa Kusini Pemba.

Matembezi hayo ya kihistoria yalianzia Bandarini Mkoani, yakapitia maeneo ya Mtuhaliwa, Chanjamjawiri, na kuhitimishwa katika Gombani ya Kale, yakihusisha vijana kutoka makundi mbalimbali wakiwa wamevalia mavazi ya kizalendo ya Chama Cha Mapinduzi, wakiwa na mabango, bendera na nyimbo za kizalendo zilizoakisi historia, mshikamano na dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akiongoza matembezi hayo, Mwenyekiti Kawaida ameonesha kwa vitendo nafasi ya vijana katika kulinda, kutetea na kuenzi misingi ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar—Mapinduzi yaliyoasisiwa Januari 12, 1964, yakileta usawa, haki ya kijamii, utu na mamlaka ya wananchi wa Zanzibar.

Baada ya kukamilika kwa matembezi hayo, Mwenyekiti Kawaida anatarajiwa kuzungumza na wanamatembezi, ambapo atatoa ujumbe maalum wa kuhitimisha matembezi hayo, ikiwa ni siku ya mwisho ya matembezi ya maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi katika mikoa ya Pemba. Ujumbe huo unalenga kuwakumbusha vijana wajibu wao wa kihistoria katika kuilinda amani, mshikamano wa kitaifa, na kuendeleza kazi na utu kama msingi wa maendeleo ya Taifa.

Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanaendelea kuwa chachu ya kuimarisha uzalendo, kuenzi mashujaa wa Mapinduzi, na kuimarisha mshikamano wa Watanzania, hususan vijana, katika kujenga Zanzibar na Tanzania yenye maendeleo, haki na usawa kwa wote.