UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

KATIBU MKUU CCM DKT. ASHA ROSE MIGIRO: MABALOZI WA MASHINA NDIO SAUTI HALISI YA CHAMA

07 Jan, 2026 59 Machapisho
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha Rose Migiro, amewataka Mabalozi wa mashina kote nchini kuwa viongozi wenye uthubutu, dira na sauti, wasiobaki kuwa wapokeaji wa maelekezo kutoka juu pekee, bali wawe chimbuko la mawazo, maamuzi na maelekezo yanayopanda kutoka chini kwenda juu, kwani wao ndiyo wanaoishi na kuwatambua kwa karibu wanachama wa CCM.

Dkt. Migiro ametoa wito huo leo, tarehe 7 Januari 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kuanza kwa ziara yake ya kikazi ya kukutana na kuzungumza na Mabalozi wa mashina, ambapo ameanza na Wilaya za Temeke na Kigamboni, hatua inayoonesha dhamira ya dhati ya uongozi wa chama kushuka chini na kusikiliza sauti ya msingi ya wanachama.
Akizungumza mbele ya maelfu ya Mabalozi wa mashina, Katibu Mkuu huyo ametumia jukwaa hilo kutoa shukrani za dhati kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Itikadi, Uenezi na Mafunzo), Ndugu Kenani Kihongosi, akimtaja kuwa mlezi mahiri wa kichama wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliyeendelea kutoa nasaha, maelekezo na hamasa kwa viongozi wa ngazi zote kwa kusisitiza mfumo wa uongozi unaotoka chini kwenda juu.
Katika hotuba yake, Dkt. Migiro ameweka msisitizo mkubwa juu ya nafasi ya mashina na kata kama nguzo kuu za uimara na umadhubuti wa Chama Cha Mapinduzi, akibainisha kuwa nguvu ya CCM haianzi juu bali inaanzia chini kabisa kwa wanachama walioko mashinani.

Amesisitiza kuwa Mabalozi wa mashina wanapaswa kushirikiana kwa karibu, kushauriana na kujenga mshikamano wa kweli ili kutimiza malengo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha CCM inaendelea kuwa imara, thabiti na chama kinachoishi na kugusa maisha ya wananchi siku hadi siku.

Aidha, Katibu Mkuu  amewahimiza Mabalozi na viongozi wote wa CCM kurejea na kuyasimulia kwa ujasiri mambo makubwa na mazuri yaliyotekelezwa chini ya Ilani ya CCM katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, pamoja na mafanikio yaliyopatikana hata katika kipindi cha miezi miwili tangu kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu, akisisitiza kuwa historia ya utekelezaji bora wa ilani ni silaha muhimu ya kisiasa na kiitikadi.
Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Asha Rose Migiro, jijini Dar es Salaam inaendelea kuwa ishara ya uongozi unaosikiliza, unaojenga na unaothamini msingi wa chama, huku kauli na maelekezo yake yakizidi kuimarisha matumaini, ari na mshikamano miongoni mwa Mabalozi wa mashina na wanachama wa CCM kwa ujumla.