UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

DKT. MIGIRO NI CHACHU YA MATUMAINI MAKUBWA KWA VIONGOZI WA MASHINA – MWENEZI KENANI

07 Jan, 2026 61 Machapisho
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Kenani Kihongosi, amesema Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Balozi Dkt. Asha Rose Migiro, ni chachu ya matumaini makubwa kwa viongozi wa mashina na wanachama wa chama hicho kutokana na uongozi wake wa mfano, unaojikita katika kulea, kufundisha na kuwaimarisha viongozi kuanzia ngazi ya chini.
Akizungumza leo, tarehe 7 Januari 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kuanza kwa ziara ya Katibu Mkuu Dkt. Migiro ya kukutana na kuzungumza na mabalozi wa mashina kutoka Wilaya za Temeke na Kigamboni, Mwenezi Kenani ametoa pongezi zake za dhati kwa Katibu Mkuu huyo kwa kuendelea kuwa mlezi na mwalimu bora wa viongozi na wanachama wa CCM.
Amesema kuwa uongozi wa Dkt. Migiro umejengwa juu ya misingi ya malezi, mafunzo na maadili, jambo linalowafanya wanachama wa CCM kujivunia uwepo wake. Katika maelezo yake, Mwenezi Kenani amesema:
“Katibu Mkuu wetu Dkt. Migiro ni kiongozi wa mfano. Umetulea vema, umetufundisha, na pale tunapokosea umekuwa mama mlezi wetu. Tunajivunia kuwa sehemu ya uongozi wako kwa sababu umeendelea kuwa mwalimu bora ndani ya Chama Cha Mapinduzi.”
Aidha, Mwenezi Kenani amepongeza kauli mbiu ya Katibu Mkuu kwa mabalozi wa mashina isemayo ‘Shina Lako Linakuita’, akieleza kuwa kauli hiyo imekuja kwa wakati muafaka na inalenga kuamsha uhai mpya wa chama kuanzia ngazi ya shina, ambayo ndiyo msingi na nguzo kuu ya CCM.
Amesisitiza kuwa msisitizo wa kushuka chini na kutembelea mashina unaonesha dhamira ya dhati ya Katibu Mkuu ya kufanya mageuzi chanya ndani ya CCM na jumuiya zake, akibainisha kuwa hilo ni jambo la heshima kubwa kwa viongozi wa mashina na mabalozi wao.
“Kauli mbiu hii ya ‘Shina Lako Linakuita’ inathibitisha dhamira yako ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Mashina ndiyo mali, msingi na nguzo ya CCM, na kuyatambua na kuyapa heshima ni kulijenga chama kwa misingi imara,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Mwenezi Kenani amewahimiza Watanzania wote kuendelea kuilinda amani ya Taifa kwa wivu mkubwa, akisisitiza kuwa amani hiyo ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Ameongeza kuwa Tanzania imebahatika kuwa na Rais Mwanamama mwenye upendo, busara na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuendelea kuleta maendeleo kwa Taifa kwa ujumla.
Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asha Rose Migiro, jijini Dar es Salaam inaendelea kuonekana kama jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano wa chama, kuwasikiliza mabalozi wa mashina na kujenga dira mpya ya utendaji inayolenga kuimarisha CCM kuanzia ngazi ya chini kabisa.