UVCCM
Tafadhali subiri...
UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)

VIJANA VYUONI GOMBEENI UONGOZI UVCCM

05 Jan, 2026 109 Machapisho

Dodoma, 03 Januari 2026 – Katibu Msaidizi wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa, Vyuo na Vyuo Vikuu wa UVCCM, Ndugu Mabula Marco Mabula, amewahimiza vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaosoma katika vyuo na vyuo vikuu nchini kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Seneti za Vyuo na Vyuo Vikuu kupitia jumuiya ya UVCCM.

Akizungumza katika Ofisi za Makao Makuu ya UVCCM, Tambuka Reli jijini Dodoma, Mabula amesema fomu za kugombea zitatolewa kuanzia Jumatatu tarehe 05 hadi 07 Januari 2026 katika ofisi za Makatibu wa UVCCM wa mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Nafasi Zinazogombewa

Mabula ameeleza kuwa nafasi zitakazogombewa katika Seneti za Vyuo na Vyuo Vikuu ngazi ya mkoa ni pamoja na:

  • Mwenyekiti wa Seneti Mkoa
  • Katibu wa Seneti Mkoa
  • Katibu Hamasa wa Seneti Mkoa
  • Wajumbe wawili wa Kamati ya Uratibu ya Seneti Mkoa

Aidha, kutachaguliwa wajumbe watatu (3) kutoka kila wilaya wanaotoka katika matawi ya vyuo na vyuo vikuu, ambao watawakilisha katika Baraza la UVCCM katika wilaya husika kote Tanzania Bara na Zanzibar.

Sifa za Waombaji

Akizungumza kuhusu sifa za waombaji, Mabula amebainisha kuwa mgombea anatakiwa:

  • Awe mwanachama wa CCM na UVCCM
  • Awe mwanafunzi wa chuo cha kati au chuo kikuu
  • Awe amebakiza angalau miaka miwili ya masomo

Sifa nyingine zimeainishwa katika Kanuni ya UVCCM ya mwaka 1978, toleo la 2025.

Wito kwa Vijana

Mabula ametoa wito kwa vijana wote wanaokidhi vigezo hivyo kutumia fursa hiyo kujenga uwezo wao wa kiuongozi na kushiriki kikamilifu katika harakati za jumuiya, akisisitiza kuwa UVCCM ni jukwaa muhimu la kukuza na kuandaa viongozi wa baadaye wa chama na taifa.

Ziara ya Mafunzo UDOM

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa ziara ya mafunzo ya Tawi la CHSS, IDS na CI–UDOM, ambalo lilitembelea Makao Makuu ya UVCCM likiwa na wanachama wapya zaidi ya 100.

Katika ziara hiyo, wanachama hao walipata fursa ya kujifunza historia ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM na Chama Cha Mapinduzi, pamoja na kukabidhiwa kadi za uanachama.

Ziara hiyo imetajwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa UVCCM wa kuimarisha uelewa wa misingi ya chama, kuongeza uanachama, na kuhamasisha ushiriki mpana wa vijana wa vyuo katika uongozi na ujenzi wa chama.